Kitabu cha Danieli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kitabu cha Danieli ni kimojawapo kati ya vitabu vya Tanakh yaani Biblia ya Kiebrania ambamo kimo katika kundi la tatu na la mwisho, Ketuvim). Awali kiliandikwa katika lugha mbili: Kiebrania na Kiaramu. Kimepokea jina lake kutokana na mhusika wake ambaye ni Danieli, ilhali kinasimulia habari zake katika milango 6 ya kwanza halafu maono yake Danieli katika milango 7-12.

Wakristo wengi wanafuata tafsiri ya Septuaginta yenye nyongeza mbalimbali kwa lugha ya Kigiriki na kukipanga kati ya vitabu vya manabii baada ya Kitabu cha Ezekieli katika Biblia ya Kikristo.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Maana ya jina[hariri | hariri chanzo]

Tafsiri ya kawaida ya jina la mhusika mkuu, Danieli mwenye hekima, ni Mungu ni hakimu wangu.

Habari za Danieli[hariri | hariri chanzo]

Kadiri ya kitabu, Danieli alipokuwa kijana alipelekwa uhamishoni Babuloni, ambako hekima yake ya pekee ilimvutia mfalme Nebukadneza II na kumpatia cheo katika ikulu.

Sifa yake ilimwezesha kuendelea na cheo chake hata baada ya mji huo kutekwa na Wamedi na Waajemi (539 KK), ambapo alipendwa hasa na mfalme Dario[1] ingawa alikataa amri zilizokwenda kinyume cha imani na maadili ya Torati ya taifa lake, Israeli.

Mtu mwenye hekima aitwaye Danieli alitajwa mapema hata nje ya Biblia katika eneo la Mashariki ya Kati.

Wataalamu wengi wa Biblia siku hizi hawakubali habari hizi kuwa za kihistoria kutokana na makosa mengi kuhusu watu na matukio.

Vilevile hawakubali matabiri yake kuwa za kinabii, kwa maana kitabu kinaonekana kimeandikwa na watu mbalimbali na nyakati mbalimbali hadi kikakamilika katika karne ya 2 K.K. kilipokusudiwa kutegemeza Wayahudi washike kama yeye msimamo katika dhuluma za mfalme Antioko Epifane zilizowakabili kama vinavyoeleza vitabu vya Wamakabayo.

Kwa sababu hiyo mtindo wake ni wa kiapokaliptiko, kama vitabu vingi vya wakati huo, kuanzia sehemu za Ezekieli hadi kitabu cha Ufunuo

Mgawanyo wa kitabu[hariri | hariri chanzo]

Sura sita za kwanza zinasimulia hadithi za maisha ya Danieli.

Sura sita zinazofuata zinaleta njozi nyingi za usiku.

Sura za 13 na 14 ni sehemu za nyongeza kati ya Deuterokanoni.

Ujumbe[hariri | hariri chanzo]

Kwa Wakristo ni muhimu hasa maneno ya kitabu juu ya Mwana wa Adamu, jina la mtu wa kimbingu lililotumiwa sana na Yesu kujitambulisha.

Vilevile ni muhimu fundisho lake la wazi kuhusu ufufuko wa watu wote na hali mbili tofauti za milele zitakazokana na hukumu juu yao. Ni hatua ya maana katika maendeleo ya ufunuo kuhusu vikomo vya binadamu.

Sala katika sehemu za Kigiriki[hariri | hariri chanzo]

Sala ya Azaria (Dan 3:37-40)[hariri | hariri chanzo]

"Sisi, Ee Bwana, tumekuwa duni kuliko maìtaifa mengine yote, na kudhulumiwa leo katika ulimwengu wote kwa sababu ya dhambi zetu. Sasa hakuna mfalme wala nabii wala kiongozi; hakuna dhabihu wala kafara wala sadaka wala uvumba, wala mahali pa kukutolea dhabihu na kuona rehema. Lakini kwa moyo uliovunjika na kwa roho nyenyekevu tukubaliwe nawe, na sadaka yetu iwe machoni pako leo kama dhabihu za kondoo waume na ng’ombe, na kama kondoo wanono elfu kumi. Nasi tukufuate kwa unyofu, maana wanaokutumaini Wewe hawataaibika".

Sala za vijana watatu (Dan 3:52-56)[hariri | hariri chanzo]

"Umehimidiwa, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu, wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu. lastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu, wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako. wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. Umehimidiwa utazamaye vilindi, uketiye juu ya makerubi, wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. Umehimidiwa katika anga la mbinguni, wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele".

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Dario Mmedi anayetajwa hapa hajulikani kihistoria; ni mtawala tofauti na Dario I aliyetawala baada ya Koreishi Mkuu.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.

Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kitabu cha Danieli kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.